Misri ya Kale

Piramidi ya Giza pamoja na Sphinx.
Ufalme wa Misri ya Kale mnamo 1500 KK pamoja na maeneo iliyotawala.

Misri ya Kale ni ustaarabu uliokuwepo Afrika kaskazini, sambamba na mto Naili, kuanzia kwenye delta au mdomo wa Naili, toka kaskazini mwa Misri kwenda kusini hadi Jebel Barkal, kwenye maporomoko ya nne, wakati wa kupanuka kwake (Karne ya 15 KK).

Ustaarabu huo ulidumu kwa karibu milenia tatu, toka takribani mwaka 3200 KK hadi mwaka 30 KK nchi ilipovamiwa na Waroma na kuwa sehemu ya Dola la Roma. Historia ya kisiasa hutazamwa kuanza na Farao Menes mnamo 3200 KK na kwisha na uvamizi wa Wagiriki chini ya Aleksander Mkuu mnamo 332 KK. Kinachofuata kilikuwa kipindi cha Misri kama nchi ya kujitegemea chini ya mafarao Wagiriki (nasaba ya Ptolemaio) hadi kuvamiwa na Waroma na kuwa jimbo la Dola la Roma.

Uti wa mgongo wa Misri ya Kale ulikuwa mto Naili. Sehemu kubwa ya nchi hiyo ni jangwa lakini umwagiliaji wa mashamba kwa njia ya maji ya mto huo ulileta mazao mazuri yaliyolisha watu wengi.

Mahitaji ya kupanga na kutunza mifereji pamoja na mitambo ya umwagiliaji na kusimamia ugawaji wa maji yalisaidia kutokea kwa vyanzo vya hisabati na mwandiko. Mwandiko wa Misri ulikuwa hiroglifi zilizokuwa aina ya mwandishi wa picha.

Dini ya Misri ilitarajia maisha baada ya kifo ambayo yanapaswa kuandaliwa na watu wakati wa maisha haya.

Wafalme, walioitwa Mafarao, walijengewa makaburi makubwa sana na piramidi zao ni kati ya makaburi makubwa kabisa duniani.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne