Mitaguso ya kiekumene


Mitaguso ya kiekumene (kutoka Kigiriki oικουμένη oikumene yaani dunia inayokaliwa na watu) ni jina la mikutano saba ya maaskofu wa kanisa la karne za kwanza wakati wa Mababu wa Kanisa iliyofanyika kati ya mwaka 325 hadi 787.

Mikutano hiyo ilitoa maamuzi ya kudumu juu ya mafundisho ya imani ya Kikristo yaliyokuwa muhimu kwa maendeleo ya Ukristo ya baadaye.

Yote ilitokea katika mashariki ya Dola la Roma iliyoendelea baadaye kama Milki ya Bizanti.

Mitaguso hiyo saba inakubaliwa na Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiorthodoksi, na pia katika madhehebu mengi ya Uprotestanti hasa Anglikana, Walutheri, Wamethodisti, Wamoravian na mengine.

1. Mtaguso wa kwanza wa Nikea (mwaka 325)

2. Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381)

3. Mtaguso wa Efeso (431)

4. Mtaguso wa Kalsedonia (451)

5. Mtaguso wa pili wa Konstantinopoli (553)

6. Mtaguso wa tatu wa Konstantinopoli (680-681)

7. Mtaguso wa pili wa Nikea (787)

Makanisa ya Waorthodoksi wa mashariki hukubali mitaguso mitatu ya kwanza tu. Madhehebu mengine ya Kiprotestanti yanakubali maazimio ya mitaguso kadiri yanavyolingana na uelewa wao wa Biblia.


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne