Msasa

Kwa matumizi tofauti ya jina hili angalia Msasa (Handeni)

Karatasi za msasa zenye saizi tofauti za grit (40 (kubwa), 80, 150, 240, 600 (ndogo)).

Msasa (kwa Kiingereza: sandpaper , glasspaper) ni karatasi nzito iliyotiwa chembe za dutu kikwaruzi kama punje za mchanga, za kioo kilichosagwa au siku hizi dutu sanisi (sintetiki) kama oksidi ya alumini kwa kazi kama kulainisha uso wa ubao na metali au kuodoa rangi kwenye uso wa kitu; pia kwa kukwaruza uso ulio laini sana kabla ya kupaka rangi.

Kwa matumizi katika mashine za kuburuza zenye mwendo wa kasi dutu kikwaruzi hugundishwa kwenye msingi wa kitambaa imara.

Kimapokeo kabla ya kuingia kwa mashine mafundi katika Afrika Mashariki walitumia majani ya msasa; msasa waliita vichaka na miti yenye majani yanayofaa kuburuza na kulainisha vifaa vya ubao kama vile upinde, mishale au pini ya jembe.

Miti inayoitwa msasa ni spishi za Cordia monoica, Ficus exasperata na Trema orientali.

Wavuvi wamewahi kutumia ngozi ya papa kama msasa.

Ukubwa wa chembe kwenye msasa hutajwa kwa namba; namba ndogo kama 20 au 40 inaonyesha chembe kubwa zaidi na msasa si laini sana; namba kubwa kama 1500 inaonyesha chembe ni ndogo zaidi. Kwa Kiingereza ukubwa huitwa "grit".


From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne