Kijerumani

Hadhi ya Kijerumani katika nchi mbalimbali.
Hadhi ya Kijerumani katika nchi mbalimbali.
Nchi ambako lugha ya Kijerumani huzungumzwa.

Kijerumani (pia: Kidachi[1], kwa Kijerumani: Deutsch au (die) deutsche Sprache) ni lugha ya Kigermanik ya magharibi katika jamii ya lugha za Kihindi-Kiulaya.

Huzungumzwa hasa katika nchi za Ujerumani, Austria, Uswisi, Liechtenstein na Luxemburg.

Kuna pia wasemaji asilia katika nchi jirani za Ujerumani / Austria kama Ubelgiji, Uholanzi, Ufaransa, Denmark, Poland na Italia ya kaskazini. Nchi nyingi za Ulaya ya Mashariki zilikuwa na wasemaji wa Kijerumani lakini wengi walifukuzwa au kuondoka wakati wa vita kuu ya pili ya dunia; vikundi vimebaki hasa katika Hungaria, Romania, Uceki, Urusi na Kazakhstan.

Vikundi vidogo vya watu waliohamia katika karne za 19 na 20 wanaoendelea kutumia Kijerumani wako katika Amerika ya Kaskazini (Marekani, Kanada), Amerika Kusini (Brazil, Chile) na Afrika (hasa Namibia na Afrika Kusini).

Kijerumani huzungumzwa na watu milioni 100 katika Ulaya. Ni lugha ya pili katika Ulaya baada ya Kirusi kushinda Kifaransa na Kiingereza.

  1. Kidachi ni neno la Kiswahili cha zamani linalosikika hadi leo katika sehemu za Tanzania kwa ajili ya lugha ya Kijerumani au tabia za Wajerumani. Neno limetokana na "Deutsch" (tamka: doitsh) ambalo ni jinsi Wajerumani wenyewe wanavyojiita. Kidachi, Mdachi/Wadachi na Udachi yalikuwa maneno ya Kiswahili cha kawaida kutokana na utawala wa Kijerumani katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Tangu mwisho wa ukoloni wa Wajerumani mwaka 1918 na kuja kwa Waingereza wasemaji wa Kiswahili wamezoea zaidi majina yenye asili ya Kiingereza, yaani Kijerumani, Mjerumani/Wajerumani na Ujerumani. Mara nyingi maneno yenye "-dachi" huchanganywa na neno la Kiingereza "Dutch" linalomaanisha Waholanzi.

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Nelliwinne